Umewahi kumpenda na yeye akakupenda?
Kijana mmoja alitokea kumpenda sana dada
mmoja japokuwa yeye alikuwa akimtolea nje mara kwa mara lakini kijana hakukata tamaa
katika kutafuta bahati yake kwa dada huyo huku akiamini siku moja atafanikiwa. Siku
moja dada huyo akiwa yupo nyumbani kwake ikiwa ni siku ya jumamosi tulivu akiwa
hajaenda ofisi kwake ambapo alikuwa anafanya kazi katika kampuni moja iliyokuwa
inategeneza manukato yenye harufu nzuri mithili ya ua la walidi aliamua kumpigia simu huyu kaka na kumtaka aje
nyumbani kwake, yule kijana alifurahi sana na kuhisi kama ndoto zake zinatimia.
Akiwa nyumbani kwake dada huyo akifanya
shughuli zake ndogo ndogo za hapa na pale alikuwa amevalia kanga moja laini kutokana na hali ya hewa ya joto la Dar es
salaam. Kwa upande wa yule kijana alikuwa amefurahi sana na haraka haraka
alijiandaa kwa kuvalia nguo nzuri zenye kuleta mvuto wa mtanashati kisha kuanza
safari kuelekea kwa huyu dada njiani kaka huyu alikuwa na mawazo na akijiuliza
maswali mengi huku akiwa haamini kama yule dada amemuita nyumbani kwake au
ilikuwa ni ndoto. Alipofika, alibisha hodi na yule dada akafungua mlango huku
akionyesha tabasamu pana katika paji lake la uso lenye kuleta tamanio la mahaba.
Yule Kaka aliingia ndani huku kijasho chembaba
kikimteremka mithili ya mtu aliyekuwa anakimbia. Dada huyu alimkaribisha
vizuri, kisha yule dada akamuuliza anatumia kinywaji gani yule kaka aliitikia
kwa upole na ukarimu naomba tu maji ya kunywa huku muda wote akimtazama kwa
umakini dada huyu mrembo, aliyeumbika kila idara na ile kanga nyepesi aliyovaa
ilikuwa ikionyesha umbo zuri la mahaba liloumbika mithili ya malaika. Kaka
alikuwa akivuta pumzi kwa haraka haraka, na kusema "Nimefurahi sana, umenikaribisha nyumbani kwako ni pazuri sana."
Yule dada alitabasamu na kusema "Asante sana, nimefurahi pia umeitikia
wito wangu, samahani kwa usumbufu wangu".
Yule kaka alitabasamu huku akijisogeza
sogeza "Hakuna tatizo, usijali kabisa, mimi nipo kwa ajili yako, naimani
sasa nina...." Kabla hajamilizia kuongea yule dada alimshika mikono yake
miwili huku akimtizama machoni, kwa macho yake malegevu, mithili ya mtu
aliyekula kungu "Samahani kaka, mimi nimekuita hapa kuna jambo nataka
unishauri, nataka kujua ni zawadi gani nzuri unaweza kumpatia mwanaume unayempenda"
Kaka yule alikuwa akitetemeka na kusema "Chochote tu, zawadi ni zawadi,
alimradi kuwe na mapenzi ya kweli" Dada yule alitabasamu na kusema
"Ni kweli, mapenzi ya kweli ndiyo jambo la msingi, nitampenda maisha yangu
yote" Kaka yule akauliza "Utampenda? Nani huyo"
Yule dada alitabasamu tena na
kusema "Samahani, rafiki yangu nilikuwa sijakuambia siku nyingi, wiki
ijayo nafunga ndoa na mpenzi wangu wa muda mrefu ambaye nampenda sana, na pia
nilikuita ili nikupe kadi ya harusi, nitafurahi kukuona, kwani wewe ni rafiki
yangu pia" Yule kaka alibaki amepigwa na butwaa, "Ati, nini unaolewa,
daaah, jamani, kwahiyo." Alinyanyuka na kuondoka bila ya kuaga huku
akimuacha yule dada anamuita ili ampatie kadi bila ya mafanikio.