Dar es Salaam. Migogoro ya ardhi inayojitokeza kwa sasa katika jamii imeendelea kuwa tishio la amani ya nchi yetu kutokana na athari mbalimbali zinazodaiwa kuchangiwa na matokeo ya udhaifu wa kimfumo, ongezeko la idadi ya watu, shughuli za uwekezaji, upanuzi wa miji, shughuli za ufugaji na nyinginezo nyingi.
Athari hizo zimesababisha watu kupoteza makazi, mifugo na mauaji ya kikatili kutokana na vita kati ya wakulima na wafugaji, wanavijiji na wawekezaji na wengineo, wakigombania umilliki wa ardhi katika eneo moja.
Aidha, takwimu zinaonyesha kwamba kati ya hekta milioni 80 za ardhi ya kilimo nchini, ni asilimia 10 ndiyo iliyopimwa katikati ya ongezeko la Watanzania milioni 45.
Hatua hiyo inaweza kuwa sababu ya kuwapo kwa zaidi ya kesi 6,000 za migogoro ya ardhi zinazoendeshwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania kote nchini.
Katika kushughulikia changamoto hiyo, Serikali kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria ikaingia kwenye mchakato wa kuandaa ripoti inayohusu migogoro ya ardhi nchini ili kutoa nafasi ya kufanyiwa marekebisho Sheria ya Ardhi huku ikiwashirikisha wadau wote ikiwamo, mahakama, Wizara ya Ardhi, wananchi na wanasheria.
Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande anasema ili kumaliza migogoro hiyo nchini kwa sasa ni lazima kila kesi husika iangaliwe msingi wake kwa kuzingatia inapatikana katika ngazi gani kwani migogoro mingi ipo katika ngazi za chini.
Hata hivyo, wakati harakati hizo zikiendelea, wanasiasa wamekuwa wakionekana kuingilia kati migogoro hiyo huku wakituhumiwa kulinda masilahi yao kisiasa pasipo kujali hatima ya wananchi ambao wamekuwa wakiendelea kuathirika zaidi.
Ofisa Mradi wa Haki Ardhi, Cuthbert Tomito anasema wanasiasa, hususan wabunge waliozungukwa na migogoro ya ardhi wamekuwa wakipotosha wananchi, hatua ambayo inasababisha kuchochea machafuko.
“Katika hatua za kutatua migogoro kuna mambo yanayoamuliwa kitaalamu, wakati mwingine wananchi wanaweza kuwa na makosa lakini wanasiasa wanaingilia kati kuwalaghai, kuwatia moyo matokeo yake wananchi wanafikia hatua ya kukosa uvumilivu wakiamini wana haki kumbe sivyo,” anasema Tomito na kuongeza:
“Wanasiasa wanapokuwa tayari wameingilia migogoro hiyo, upande wa watendaji ambao ni maofisa ardhi wanakosa nguvu ya kutekeleza majukumu yao, kwa hivyo ningewashauri katika hatua za kushughulikia migogoro hiyo, ni vyema wakaachia watendaji kwani wao wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria.”
Tomito anaongeza kuwa watendaji wanatakiwa kuachiwa nafasi yao wafanye kazi na wasiingiliwe kwa sababu sheria haina upindishwaji.
“Mtendaji ana uhuru mkubwa katika majukumu yake pengine tofauti na mwanasiasa ambaye anahofia kutofautiana mtazamo na wapigakura wake,” anasema.
Source: Mwananchi