Afrika Kusini imewatuhumu
wanadiplomasia watatu wa Rwanda waliofurushwa kutoka nchini humo kwa kuhusika
na mauaji na njama ya mauaji dhidi ya wapinzani wa serikali ya Rwanda wanaoishi
Afrika Kusini.
Waziri
wa sheria wa Afrika Kusini, Jeff Radebe amesema kuwa ana ushahidi wa kutosha
unaowahusisha watatu hao na vitendo vyinavyokiuka sheria.
Wanadiplomasia
hao, walifurushwa siku ya Ijumaa baada ya kutokea uvamizi nyumbani kwa Generali
Kayumba Nyamwasa aliyekuwa wakati mmoja mwandani wa Rais Kagame, mjini
Johannesburg.
Rwanda
ambayo nayo iliwafurushwa wanadiplomasia sita wa Afrika Kusini kutoka mjini
Kigali, imekanusha madai ya kuhusika na njama hiyo.
Msemaji
wa Bwana Radebe, Mthunzi Mhaga, aliambia BBC kuwa uchunguzi ulibaini kuwa
watatu hao walihusika na uvamizi huo na mashambulizi mengine dhidi ya watu
wanaoonekana kuwa wapinzani wa serikali ya Rwanda wanaoishi nchini Afrika
Kusini.
Watu
waliokuwa wamejihami, walivamia nyumba ya Luteni Generali Nyamwasa, mkuu wa
zamani wa majeshi ya Rwanda wiki jana lakini hakuwepo nyumbani wakati wa
uvamizi huo.
Wavamizi
hao walifanya msako ndani ya nyumba hiyo na kuondoka wakiwa wamebeba Komputa na
stakabadhi kadhaa. Generali Nyamwasa ameponea majaribio mawili ya kumuua
ikiwemo kupigwa risasi mjini Johannesburg mwaka 2010 baada ya kutoroka Rwanda.
Alitafuta
hifadhi nchini Afrika Kusini baada ya uhusiano wake na Kagame kuvunjika. Januari
mwaka huu mwili wa aliyekuwa jasusi mkuu wa Rwanda, Patrick Karegeya,
ulipatikana ndani ya hoteli moja mjini Johannesburg akiwa na alama za
kunyongwa.
Maafisa
wa zamani wa serikali ya Rwanda waliokimbilia usalama wao katika nchi za
Magharibi ikiwemo Uingereza na Marekani wanasema kuwa maafisa wa usalama wa
serikali wametishia kuwaua.
Muda
mfupi baada ya kifo cha Karegeya Rais Kagame alionya kuwa wale ambao wanasaliti
nchi hiyo watakiona cha mtema kuni.
Afrika
Kusini ilikuwa wakati mmoja mshirika mkubwa wa Afrika Kusini na hata kununua
silaha kutoka kwake, lakini uhusiano kati ya nchi hizo umeendelea kuzorota kila
kukicha kufuatia mashambulizi dhidi ya waliokuwa maafisa wa Rwanda
waliokimbilia nchini humo.
Source: BBC Swahili