Watoto wanaodaiwa kufanyiwa ukatili wakionyesha vidonda kwenye mikono yao ambavyo vinatokana na kuchomwa moto na baba ya mzazi nyumbani kwao Mbagala Kibondemaji jijini Dar es Salaam jana.
Vitendo
vya ukatili dhidi ya watoto vinavyofanywa na baadhi ya wazazi, vimezidi
kukithiri nchini baada ya watoto wawili kudaiwa kuchomwa moto mikono na
baba
yao kwa kutumia tambi za jiko jijini Dar es Salaam. Katika tukio hilo,
anayetuhumiwa kufanya unyama huo ni Salum Juma, fundi gereji wilayani
Temeke, mkazi wa Mbagala Kibonde Maji, jijini Dar es Salaam.
Watoto
hao mmoja mwenye umri miaka saba na mwingine miaka mitano (majina yao
yamehifadhiwa), akiwamo wa kumzaa na wa kufikia walikutwa na mkasa huo
baada ya kwenda kuangalia runinga kwa jirani na kurudi nyumbani saa 5:00
usiku Alhamisi wiki iliyopita.
Akizungumza
na NIPASHE, jirani yao, Omar Fusi, alidai watoto hao walieleza kuwa
walichomwa na baba yao na kufichwa ndani, lakini baadaye majirani
waliwaona watoto hao wakiwa na majeraha.
Fusi alisema baada ya
kuwaona wakiwa na majeraha, waliwahoji ambapo walieleza kuwa walichomwa
na baba yao baada ya kuchelewa kurudi kutoka kuangalia televisheni.
Kwa mujibu wa Fusi, kitendo hicho kilifanyika huku mama yao akiwa kwenye biashara zake za kukaanga mihogo.
Fusi
alisema baada ya kubaini tukio hilo alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Kibonde Maji ‘B’, Teofile Balae, ambaye alitoa
taarifa kwa Ofisa Ustawi wa Jamii kata ya Mbagala, Eliameresa Kaaya na
kuripoti polisi na kufanikisha baba huyo kukamatwa na kupelekwa katika
Kituo cha Polisi Maturubai ambako anaendelea kushikiliwa.
Balae
alisema baada ya kushirikiana na Ofisa Ustawi wa Jamii na baba huyo
kukamatwa, waliwachukua watoto hao na kuwapeleka Kituo cha Polisi
Mbagala Kuu kwa ajili ya kupata fomu ya PF3 na kuwapeleka katika
hospitali ya Mbagala Rangi Tatu kupatiwa matibabu.
Mmoja
wa wakazi wa eneo hilo, Erasto Kibara, alisema walibaini watoto hao
kufanyiwa ukatili huo baada ya kumkuta mmoja wao adukani alikotumwa
akiwa na majeraha na kumuuliza kilichompata kisha alitoa taarifa hizo
kwa mwenyekiti wa mtaa huo.
Ofisa
Ustawi wa Jamii, Kaaya, akizungumza na NIPASHE katika Kituo cha Polisi
Maturubai wakati watoto hao wakichukuliwa maelezo na polisi, alisema
kitendo walichofanyiwa watoto hao ni cha kikatili na kuwataka wananchi
kutoa taarifa pale wanapogundua ukatili katika mitaa yao ili kutokomeza
vitendo hivyo vilivyoshika kasi nchini.
NIPASHE
iliwashuhudia watoto hao katika Kituo cha Polisi Maturubai huku wakiwa
na majeraha mkononi wakati wakichukuliwa maelezo na maofisa wa polisi wa
kituo hicho.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mbagala Rangi Tatu, Dk. Julius
Nyakazilibe, alithibitisha watoto hao kupokelewa hospitalini hapo na
kupatiwa huduma ya matibabu kutokana na majeraha yaliyosababishwa na
moto.
“Ni
kweli watoto hao tuliwapokea hapa hospitalini wakiwa na Ofisa Ustawi wa
Jamii na walipatiwa matibabu,” alisema Dk. Nyakazilibe. Mama mzazi wa
watoto hao, Christina
Menasi, akiwa katika kituo cha polisi na mtoto wake mchanga huku
akimnywesha uji, alisema wakati wa tukio hilo, alikuwa katika biashara
yake ya kuchoma mihogo na aliporudi nyumbani na kukuta hali hiyo,
aliingiwa na hofu ya kuripoti tukio hilo kwa kumhofia mumewe.
Mama huyo alilaani kitendo hicho cha kikatili lakini alisema akifungwa yeye ndiye atakuwa na mzigo mkubwa wa kulea familia hiyo.
“Inatakiwa
tuache vitendo hivi vya kikatili, lakini ikiwa mume wangu atafungwa,
mimi ndiye nitakayebeba mzigo wa kulea hii familia,” alisema Christina.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kihenya Kihenya, alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa anashikiliwa katika Kituo cha Polisi
Maturubai na kwamba upelelezi unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani
ili sheria ichukue mkondo wake.
CHANZO: NIPASHE