Misaada hiyo ina nia ya kuboresha mazingira
ya kukabiliana na kasi ya China.
Waziri Mkuu wa Japani, Shinzo Abe ameahidi
kutoa msaada wa Dola 32 bilioni kwa Afrika katika kipindi cha miaka mitano
kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia sekta za serikali na binafsi.
Abe ametoa ahadi ya masaada huo wakati wa
ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa siku tatu kuhusu maendeleo ya Afrika
unaofanyika katika Mji wa Yokohama nchini Japani.
Msaada huo unajumuisha utoaji wa Yeni 650
bilioni kwa ajili ya mikopo katika ujenzi wa miundombinu na mpango wa mafunzo
kwa ajili ya vijana wa Afrika.
Abe alisema kuendeleza rasilimali ya nguvu
kazi, huduma muhimu za matibabu na kukuza sekta ya kilimo ni mambo muhimu katika
kuchochea ukuaji wa uchumi wa Afrika.
Alisema kile inachokihitaji Afrika ni
uwekezaji katika sekta binafsi ambapo ushirikiano kati ya sekta za umma na
binafsi utatoa fursa ya kufaidikia na uwekezaji huo.
Tangazo lake hilo linaonyesha shauku ya
Japani kuchuana na China katika kuipatia msaada na kuwekeza Afrika, bara lenye
utajiri wa maliasili.
Licha ya uhusiano wa muda mrefu uliopo kati
ya Japani na Afrika, umuhimu wa Japan kwa bara hilo umekuwa ukipungua
kulinganishwa na ule wa China ambapo kiwango chake cha biashara na Afrika
ikilinganishwa na Japan ni mara tano zaidi na mara nane zaidi katika uwekezaji
wa moja kwa moja.
China huwa haitangazi kiwango cha msaada
wake wa maendeleo lakini ripoti zinadokeza kwamba hutoa hadi dola bilioni mbili
kila mwaka.
Kiwango ilichotangaza Japani Jumamosi
kimepita sana kiwango hicho cha China.
Uhusiano wa Japani kwa Afrika unatofautiana
na mataifa mengine kwa bara hilo, alisema Abe katika kauli inayoonekana
kuikusudia China
Mpango huo utawapa fursa vijana 1,000 wa
Kiafrika kujifunza katika vyuo vikuu vya Japani na kujifunza kazi katika
kampuni za Kijapani.
No comments:
Post a Comment