Monday, 25 April 2016

PENZI LA MVUTO


Umewahi kumpenda na yeye akakupenda?
Kijana mmoja alitokea kumpenda sana dada mmoja japokuwa yeye alikuwa akimtolea nje mara kwa mara lakini kijana hakukata tamaa katika kutafuta bahati yake kwa dada huyo huku akiamini siku moja atafanikiwa. Siku moja dada huyo akiwa yupo nyumbani kwake ikiwa ni siku ya jumamosi tulivu akiwa hajaenda ofisi kwake ambapo alikuwa anafanya kazi katika kampuni moja iliyokuwa inategeneza manukato yenye harufu nzuri mithili ya ua la walidi  aliamua kumpigia simu huyu kaka na kumtaka aje nyumbani kwake, yule kijana alifurahi sana na kuhisi kama ndoto zake zinatimia. 

Akiwa nyumbani kwake dada huyo akifanya shughuli zake ndogo ndogo za hapa na pale alikuwa amevalia kanga moja laini  kutokana na hali ya hewa ya joto la Dar es salaam. Kwa upande wa yule kijana alikuwa amefurahi sana na haraka haraka alijiandaa kwa kuvalia nguo nzuri zenye kuleta mvuto wa mtanashati kisha kuanza safari kuelekea kwa huyu dada njiani kaka huyu alikuwa na mawazo na akijiuliza maswali mengi huku akiwa haamini kama yule dada amemuita nyumbani kwake au ilikuwa ni ndoto. Alipofika, alibisha hodi na yule dada akafungua mlango huku akionyesha tabasamu pana katika paji lake la uso lenye kuleta tamanio la mahaba. 

Yule Kaka aliingia ndani huku kijasho chembaba kikimteremka mithili ya mtu aliyekuwa anakimbia. Dada huyu alimkaribisha vizuri, kisha yule dada akamuuliza anatumia kinywaji gani yule kaka aliitikia kwa upole na ukarimu naomba tu maji ya kunywa huku muda wote akimtazama kwa umakini dada huyu mrembo, aliyeumbika kila idara na ile kanga nyepesi aliyovaa ilikuwa ikionyesha umbo zuri la mahaba liloumbika mithili ya malaika. Kaka alikuwa akivuta pumzi kwa haraka haraka, na kusema "Nimefurahi sana, umenikaribisha nyumbani kwako ni pazuri sana." Yule dada alitabasamu na kusema "Asante sana, nimefurahi pia umeitikia wito wangu, samahani kwa usumbufu wangu".

Yule kaka alitabasamu huku akijisogeza sogeza "Hakuna tatizo, usijali kabisa, mimi nipo kwa ajili yako, naimani sasa nina...." Kabla hajamilizia kuongea yule dada alimshika mikono yake miwili huku akimtizama machoni, kwa macho yake malegevu, mithili ya mtu aliyekula kungu "Samahani kaka, mimi nimekuita hapa kuna jambo nataka unishauri, nataka kujua ni zawadi gani nzuri unaweza kumpatia mwanaume unayempenda" Kaka yule alikuwa akitetemeka na kusema "Chochote tu, zawadi ni zawadi, alimradi kuwe na mapenzi ya kweli" Dada yule alitabasamu na kusema "Ni kweli, mapenzi ya kweli ndiyo jambo la msingi, nitampenda maisha yangu yote" Kaka yule akauliza "Utampenda? Nani huyo"


Yule dada alitabasamu tena na kusema "Samahani, rafiki yangu nilikuwa sijakuambia siku nyingi, wiki ijayo nafunga ndoa na mpenzi wangu wa muda mrefu ambaye nampenda sana, na pia nilikuita ili nikupe kadi ya harusi, nitafurahi kukuona, kwani wewe ni rafiki yangu pia" Yule kaka alibaki amepigwa na butwaa, "Ati, nini unaolewa, daaah, jamani, kwahiyo." Alinyanyuka na kuondoka bila ya kuaga huku akimuacha yule dada anamuita ili ampatie kadi bila ya mafanikio.

1 comment:

Unknown said...

500-1000 के नोट बंद होने से चमका गोल्ड, 400 रुपये प्रति ग्राम महंगा
Read more todaynews18.com https://goo.gl/HKU1t0