Kengele ya kutoka darasani iligongwa, wanafunzi wa shule
ya msingi wakaanza kutoka madarasani huku wakifukuzana wengine wakipiga kelele
ilimradi shwangwe tu.Ilikuwa mara yangu ya kwanza kufundisha shule za hatua
hiyo. Ilikuwa ni shule ya serikali.
Jicho langu liliangukia katika sura ya msichana mdogo,
nguo zake chafu. Alikuwa analia. Alikuwa peke yake
na hakuwa na yeyote wa kumbembeleza. Mimi kama mwalimu
sikutaka kujisogeza karibu naye sana. Kwanza nilikuwa mgeni. Nikaachana naye.
Siku iliyofuata tukio kama lile likajirudia. Msichana
yuleyule wakati ule uleule wa kutawanyika, alikuwa analia sana. Mwishowe
aliondoka huku akiwa analia.
“Mbona mwenzenu analia?” nilimuuliza mwanafunzi mmoja.
“Huyo ni mama kulialia..” alinijibu huku anacheka.
Haikuniingia akilini hata kidogo kuwa yule binti analia
bila sababu.
Siku ya tatu nikaanza kujiweka karibu naye.
Muda wa mapumziko nilimwita nikamnunulia chai, alikuwa
ananiogopa na hakutaka kuniangalia machoni.
Sikumuuliza lolote juu ya tabia yake ya kulia lia kila
anaporuhusiwa kurejea nyumbani.
Hata siku hiyo pia alilia vilevile. Wenzake wakawa
wanamzomea. Akili yangu iligoma kuamini kuwa binti yule analia bila
sababu. Kwanini alie wakati wa kutawanyika tu?? Hapana si bure. Nikaendelea kujiweka
karibu naye. Mkuu wa shule akafikishiwa taarifa kuwa nina mahusiano ya
kimapenzi na yule mtoto.
Moyo wangu na Mungu pekee ndio walikuwa mashahidi.
Nilikosa cha kujibu.
Nilijaribu kujiweka mbali naye lakini moyo ulinambia kuwa
kuna jambo natakiwa kulijua. Nikaendelea kuwa
karibu naye. Hatimaye mkuu wa shule akanisimamisha kufundisha pale kwa tabia
yangu ya kufanya mapenzi na mwanafunzi.
Nilijitetea lakini sikueleweka. Nikamwachia Mungu……
Licha ya kusimamishwa kazi, niliendelea kufuatilia nyendo
za yule binti aliyeitwa Janeth. Kila alipotoka
shule nilimvizia njiani na kumnunulia chakula, kisha tunazungumza kidogo.
Aliponiamini kama kaka yake ndipo nikajieleza dukuduku
langu.
“Janeth…” nilimuita.
“Bee kaka ….” Aliitika huku akinitazama.
“Nyumbani unaishi na wazazi.”
“Ndio naishi na mama..baba huwa anasafiri safari.”
“Mama yako ana watoto wangapi?”
“Mama yangu alikufa….alikufa nikiwa mdogo hata simkumbuki”
Alijibu kwa sauti ya chini.
“Kwa hiyo unaishi na mama mdogo.”
“Ndio.”
“Unampenda mama mdogo?”
Swali hili likaikatisha furaha ya Janeth. Akaanza kulia,
alilia bila kukoma, Janeth alilia kwa uchungu hadi nikajisikia vibaya.
Nilimbembeleza kisha sikumuuliza tena. Siku zikaenda bila
kumuuliza chochote..
Baada ya siku kumi, ilikuwa siku ya michezo pale shuleni,
hivyo hapakuwa na masomo. Janeth alichelewa
kuja shule, nilimngoja uwanjani, hadi alipofika majira ya saa nne.
Nikamwambia twende kunywa chai.
Siku hiyo nilimpeleka mbali kidogo, tukanywa chai, kisha
tukakaa mahali palipokuwa wazi. Nikaleta tena
mjadala mezani. Ni kuhusu maisha ya Janeth. Alikataa kabisa
kusema lolote, nilimshawishi sana. “Usiogope mimi ni
kaka yako.” Nilimpooza. Janeth badala ya kusimulia akaanza kulia tena.
“Ataniua mama nikisemaaaa” alilalamika.
Nikambembeleza hatimaye akanieleza jinsi anavyonyanyaswa
na mama yake. “Mama hanipendi hata kidogo, ananipiga na kuninyima
chakula, hapendi nije shule, vyombo tunavyotumia usiku hataki nivioshe usiku na
hataki niwahi kuamka asubuhi, nikiamka natakiwa kufanya kazi zote, kufagia
uwanja, kudeki nyumba, kuosha vyombo kisha ndipo nije shule. Baba akiwepo
anajidai kunijali sana…”
Alijieleza.
“Ni hayo tu Janeth….niambie kila kitu.”
“Akijua ananiua alisema….”
“Kwani amewahi kukutesa vipi..”
Ni hapa Janeth alivyozungumza huku analia kilio ambacho
hakitatoka masikioni mwangu kamwe.
Siku moja, alichelewa kuamka, ilikuwa siku ya mapumziko.
Mama yake alipomwamsha, aliitika na kupitiwa usingizi
tena.
Mama aliporejea mara ya pili, alikuwa na mti mkavu,
alimpiga nao kichwani na popote pale katika mwili, alipoona hiyo haitoshi
akamvua nguo, akausokomeza katika sehemu za siri, aliuigiza hovyohovyo, ukuni
huo ulikuwa wa moto.
Yeyote mwenye moyo wa nyama ajifikirie ukuni wa moto
ukazamishwa sehemu za siri za mtoto wa darasa la sita.
Nilitokwa machozi.
Nikawahi kujifuta hakuona.
“Baba yeye alisemaje….”
“Baba ni mkali na hapendi kunisikiliza na mama aliniambia
nikiambia mtu ananiua mara moja.” Alijibu kwa huzuni.
“Nikija na dada yangu tunaweza kukuona ulivyounguzwa..”
“Ndio…” alinijibu. Sikutaka kulaza
damu nikampigia simu rafiki yangu wa kike. Nikamuuliza kama
yupo kwake, alikuwepo. Nikaongozana na Janeth.
Tukafika, Janeth akatoa nguo zote.
Ilihitaji moyo wa kiuaji sana kutazama mwili wa Janeth
mara mbilimbili. Alitisha, hakika alikuwa ameunguzwa vibaya na vidonda
vilikuwa havijapona vizuri. Dada yule
alishindwa kujizuia alimlazimisha Janeth twende kwa mama yake amkabiri na kumpa
kipigo. Nikamzuia. Hata mimi nilikuwa na hasira kali. Lakini sikutaka
kuiruhusu ifanye kazi.
Nikachukua kamera, nikampiga picha Janeth katika yale
makovu.
Mbio mbio nikaenda polisi, kituo cha haki za watoto
nikaelezea mkasa ule huku nikishindwa kujizuia machozi.
Nikawaonyesha na picha. Tukaongozana nao
hadi nyumbani kwao Janeth. Mama yule
akakamatwa bila kutarajia. Nilitamani kumrukia
nimng’ate lakini haikuruhusiwa.
Sheria ikafuata mkondo. Janeth akaanza kupokea tiba.
Yule mama akahukumiwa kwenda jela miaka sita..hadi sasa
yupo jela.
Mume wake alitozwa faini kubwa kwa kosa la kutofuatilia
maendeleo ya mtoto wake kiafya…….. Mimi nilirudishwa
kazini, kwa heshima kubwa. Heshima ya nkumkomboa mtoto.
***Akina JANETH wapo mtaani kwako…..usiwaangalie na
kuwaacha tu…hebu jaribu KUWA SAUTI YAO….hawawezi kusema…hebu sema badala yao…….wanalia
kisikie kilio chao.
1 comment:
500-1000 के नोट बंद होने से चमका गोल्ड, 400 रुपये प्रति ग्राम महंगा
Read more todaynews18.com https://goo.gl/HKU1t0
Post a Comment