Rais Vladimir Putin wa Urusi
Rais
Vladimir Putin wa Urusi, amesema bado hakuna haja kwa nchi yake kupeleka
majeshi nchini Ukraine.
Bwana Putin
amesema Urusi ina haki ya kutumia njia zote kulinda raia wake walioko mashariki
mwa Ukraine
Amekanusha taarifa
kwamba majeshi ya Urusi yamewazingira raia wa Ukraine walioko katika jimbo la
Crimea, bali ni watu wanaoiunga mkono Urusi na ambao wanajilinda wenyewe.
Bwana Putin
amesema kuondolewa madarakani kwa Rais Viktor Yanukovych katika mji mkuu wa
Ukraine, Kiev ni "ukiukaji wa katiba na uporaji wa madaraka
kijeshi.".
Amesema wapiganaji
hao wameitumbukiza Ukraine katika "vurugu". Pia amesema wapigania
utaifa na wapinga usemiti wanarandaranda katika mitaa ya Kiev na miji mingine.
Amesema iwapo watu
wanaozungumza Kirusi mashariki mwa Ukraine watahitaji msaada wa Urusi, basi
Urusi itakubaliana na ombi lao.
"kama tutaona
hali hii ikianza kutokea maeneo ya mashariki, tuna haki ya kutumia kila
njia" amesema.
Bwana Putini
amesema katika jimbo la Crimea watu wenye silaha wanaoiunga mkono Urusi na raia
wamezingira kambi za kijeshi za Ukraine, sio askari wa Urusi.
"Majeshi ya
eneo hilo kwa ajili ya kujilinda" ndiyo yanayohusika na kuchukuliwa kwa
majengo ya serikali katika Crimea, amesema.
Viktor Yanukovych rais wa Ukraine aliyepinduliwa
Ukraine imesema
Urusi imepeleka maelfu ya askari katika eneo la Crimea hivi karibuni.
Uhasama
umeongezeka katika kituo cha kijeshi cha Belbek karibu na Sevastopol, mji wa
bandari ambao ni kambi ya majeshi ya majini ya Urusi.
Akizungumzia
kupinduliwa kwa Bwana Yanukovych, Bwana Putin amesema kiongozi huyo
aliyeondolewa madarakani nchini Ukraine alikubali matakwa yote ya wapinzani.
Bwana Putin
amesisitiza kuwa Bwana Yanukovych bado ni rais halali wa Ukraine.
Amesema kuna mambo
matatu ya kumwondoa madarakani rais, ameyataja kuwa ni kifo, kujiuzulu au
kushtakiwa.
Bwana Yanukovych
alikimbilia Urusi, na Bwana Putin aliwaambia waandishi wa habari:
"Sifikiri kama ana mustakabhali mwema kisiasa".
Urusi ilimsaidia
kwa sababu za "kibinadamu", amesema, "vinginevyo angekuwa
ameuawa".