Beki
wa Yanga, Juma Adbul (Kushoto) akimzuia winga wa Azam, Farid Mussa wakati wa
mechi ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la Kagame iliyofanyika kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Azam ilishinda kwa penalti 5-3. Picha na Said
Khamis.
Kwa ufupi
Yanga
imetolewa kwenye michuano ya Kombe la Kagame na timu ya Azam kwa mikwaju 5-3 ya
penati.
Dar
es Salaam. Azam imezima ndoto ya Yanga ya kutwaa taji la sita la mashindano ya
Kombe la Kagame baada ya kuitoa kwa penalti 5-3 katika mchezo wa robo
fainali uliofanyika jana kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baada
ya timu hizo kumaliza dakika 90, bila ya kufungana ndipo ilipokuja changamoto
ya mikwaju ya penalti ambayo mwaka huu imekuwa mwiba mchungu kwa Yanga ambayo
kabla ya penalti za jana tayari ilishakosa penalti tatu katika michezo ya hatua
za makundi.
Shujaa
wa Azam katika mchezo wa jana alikuwa ni kipa Aishi Manula aliyechaguliwa
mchezaji bora wa mechi baada ya kudaka penalti ya tatu ya Yanga iliyopigwa na
Haji Mwinyi.
Azam
iliyoanza kupiga penalti ilipata penalti zake zote tano zilizopigwa na Kipre
Tchetche, John Bocco, Himid Mao, Pascal Wawa na Aggrey Morris wakati kwa
upande wa Yanga waliopata ni Salum Telela, Nadir Haroub na Godfrey
Mwashiuya huku Mwinyi akikosa.
Akizungumzia
mchezo huo kocha wa Yanga, Hans Pluijm alisema ameumia kupoteza mchezo huo
ambao kwake ulikuwa kama fainali.
“Kupoteza
mchezo huu ni pigo kwangu, kwa sababu tulikuwa na malengo ya kutwaa ubingwa
katika ardhi ya nyumbani.”
Pluijm
alisema,“Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri, japo kipindi cha pili
tulitengeneza nafasi nyingi zaidi, lakini mashuti yetu mengi hayakulenga goli.
“Sasa
nguvu zetu tunaelekeza katika maandalizi yetu ya ligi inayokaribia kuanza hivi
karibuni,” alisema Mdachi huyo.
Kwa
ushindi huo sasa Azam itacheza nusu fainali Ijumaa na KCCA ukiwa kama marudiano
ya mchezo wa Kundi C ambao Azam walishinda 1-0.
Katika
mchezo wa jana timu hizo zilianza mchezo kwa kasi na kushambulia mfulululizo
tangu dakika ya kwanza ambapo Azam ilikosa bao baada ya krosi ya Shomari
Kapombe kuwapita mabeki wa Yanga, lakini John Bocco alishindwa kufunga.
Yanga
ilijibu mapigo dakika moja baadaye kupitia mshambuliaji wake Donald Ngoma
aliyewatoka mabeki wa Azam na kupiga shuti lililopanguliwa na kipa Aishi
Manula na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kipa
wa Azam, Manula alilazimika kufanya kazi ya kupangua shuti la Juma Abdul
alililopiga akiwa umbali wa mita 18 katika dakika ya 8. Pia mpira wa
kurushwa wa Mbuyu Twite nusuru uingie golini kama si ustadi wa Manula kuutoa
nje.
Yanga
iliyokuwa ikitumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao ni mabeki wanne wakisaidiwa na viungo
wawili wakabaji, viungo watatu washambuliaji na mshambuliaji mmoja, ilifanya
mashambulizi mengi kipindi cha pili.
Azam
iliyokuwa ikitumia mfumo wa 4-3-3, ambao ilitumia mabeki wanne, viungo watatu
na washambuliaji watatu, ilitumia mashambulizi ya kushtukiza na katika
dakika 34 nusura ipate bao, lakini shuti la Tchetche lilipanguliwa na kipa wa
Yanga, Mustapha ‘Barthez’ na kurudi uwanjani na kumkuta Himid Mao aliyepiga
shuti la chini na Tchetche alipojaribu kuunganisha mpira ulipaa juu.
Tofauti
na michezo iliyopita, jana washambuliaji wa Yanga, Tambwe, Ngoma,
Mwashiuya na Kaseke walikuwa kwenye wakati ngumu mbele ya ngome ya Azam
iliyoongozwa na Wawa, Morris, Kapombe na Kheri Abdallah iliyocheza kwa
maelewano makubwa kuziba njia.
Kipindi
cha pili kocha wa Azam, Stewart Hall aliwapumzisha Frank Domayo, na Kheri
Abdallah na kuwaingiza Ame Ally na Said Morad wakati Hans Pluijm aliwatoa
Kaseke, Juma Abdul, Niyonzima na kuwaingiza Salum Telela, Joseph Zutah na
Malimi Busugu.
Pamoja
na mabadiliko hayo bado timu hizo ziliendelea kutengeneza nafasi nyingi za
kufunga, lakini hakuna timu iliyofanikiwa kutumia na mchezo ukaingia katika
ubabe wa hapa na pale.
Twite
alinusurika kupewa kadi nyekundu katika dakika ya 74 baada ya kumchezea vibaya
Himid Mao wakati akiwa tayari na kadi ya njano aliyopewa dakika 71 kwa
kumchezea vibaya Mao. Pia Jean-Baptiste Mugiraneza alipewa kadi ya njano kwa
kumchezea vibaya Tambwe dakika 78.
Hadi
filimbi ya mwisho inapigwa kuashiria kumalizika kwa mechi hiyo, Azam ilikuwa
imetunza rekodi yake ya kutofungwa bao lolote hadi sasa katika mashindano hayo,
wakati Yanga ikiwa imefungwa mabao mawili.
Awali
KCCA ya Uganda ilijihakikishia kucheza nusu fainali baada ya kuichapa Al Shandy
ya Sudan kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja huo.
Mabao
ya Joseph Ochaya, Muzamir Mutyaba na Tom Masiko yalitosha kuihakikishia KCCA
kufuzu kwa nusu fainali kwa mara ya pili mfulululizo.
Mabingwa
hao wa 1978 ni mara ya kwanza katika mashindano ya mwaka huu kufanikiwa kufunga
mabao matatu kwani katika mechi zake tatu zilizopita ilifunga mabao mawili tu
No comments:
Post a Comment