Joe Biden ameonya Urusi dhidi ya kuendelea kudhibiti mji wa Crimea
Makamu wa Rais wa Marekani Joe
Biden amesema sharti Urusi ikome kuongea sana na badala yake ianze
kufanya kazi ya kusitisha mgogoro wa kisiasa nchini Ukraine.
Bwana Biden aliyasema hayo wakati wa mkutano na
waandishi wa habari ambapo waziri mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk pia
alihudhuria.
Marekani imeonya Urusi kuwa
ikiendelea kuchochea hali nchini Ukraine , itatengwa na jamii ya
kimataifa. Pia ameitaka Urusi kukomesha uungaji mkono wa vikosi vya
Ukraine vinavyounga mkono Urusi.
Joe Biden, amesema kuwa Marekani iko tayari
kuwasaidia viongozi wa Ukraine kufikia kile alichokitaja kuwa fursa ya
kihistoria ya kujenga taifa la Ukraine lenye umoja.
Biden pia aliwahutubia wabunge mjini Kiev katika
ziara iliyopangwa kuonyesha uungwaji mkono wa Marekani kwa serikali ya
mpito ya Ukraine.
Bwana Biden amesema kuwa uchaguzi wa urais uliopangwa kufanyika mwezi ujao ni muhimu zaidi katika historia ya taifa hilo.
Wakati huohuo Biden amesema kuwa Marekani
haitawai kutambua alichosema ni Udhibiti haramu wa jimbo la Crimea
ambalo linadhibitiwa na Urusi. Amesisitiza kuwa Ukraine ni nchi moja na inapaswa kusalia hivyo.
Amesihi Urusi,kuhakikisha kuwa mkataba
uliofikiwa wiki jana wa kusitisha mgogoro kwa kuamuru vikosi vya Ukraine
vinayounga mkono Urusi nchini humo kuondoka katika majengo ya serikali
waliyoyateka Mashariki mwa Ukraine.
Kadhalika Biden alisema kuwa pamoja na msaada
zaidi wa dola bilioni 50 unaodhamiria kusaidia kuchepua uchumi na kuleta
mageuzi ya kisiasa,Marekani pia inaahidi kutoa msaada wa kijeshi.
Source: BBC Swahili