Wednesday, 12 March 2014

USHIRIKISHWAJI KATIKA UAMUZI NA UTEKELEZAJI MIPANGO VIJIJINI



KUNA  wanaodhani kwamba ujamaa na kujitegemea kama sera ya kiuchumi na kuendeleza watu vijijini ni kitu kilichoshindikana na kwamba kimepitwa na wakati.
Hata hivyo, hadi wa leo hakuna kiongozi au msomi aliyekuja na siasa au sera mbadala vinavyoeleza nadharia na vitendo vipi vitumike, ili kuviondoa vijiji kwenye lindi la umaskini na kuliingiza kwenye zama za shiibe na wingi wa neema.

Pamoja na hayo, tafiti mbalimbali za watafiti na waandishi wa ndani na nje, sasa zimeanza kudhihirisha kwamba kushindwa kutekelezeka kwa siasa za ujamaa na kujitegemea nchini Tanzania, hivyo vijiji kuhukumiwa kubaki katika umaskini wa kutisha, usiopata msaada wowote wa maana kutoka Serikali kuu na wanasiasa, wakati huko Uyahudi sera kama hizo zimetumika na kuufanya mfumo na muundo wa kibuttz kuwa kitu cha kujivunia kwa kila Myahudi, kulitokana zaidi na ubinafsi wa wanasiasa na hususan viongozi.

Uoga huo kwamba ujamaa na kujitegemea, ushirikishwaji watu na watu kuchangia maendeleo yao wenyewe kuna uwezo mkubwa wa kuwapa nguvu zaidi wanavijiji, hivyo kuwatoa ujingani na kuwaweke katika nuru, ambayo itasababisha wasitawalike, wasinunuliwe, wasigawanyike na wasihadaike kirahisi ni jambo linaloendelea hadi leo.

              “ Kuna imani ya kwamba wananchi wa vijijini wakiendelea kuwa masikini, basi watawala wetu fulani wataendelea kutawala milele. Umaskini kwao umegeuka mtaji, tena mara mbili”.

Kwanza, kujihadaa kuwa wataendelea kupendwa na wanavijiji waamini kuwa wao tu ndiyo wakombozi na pili, wao kuzila fedha za misaada kwa masikini na umaskini ziku zote ukabaki palepale au kuongezeka zaidi.

Hatua ya chini kabisa katika ushirikishwaji watu katika uamuzi na utekelezaji wa mipango inayohusu maendeleo yao, inaitwa uanasesere au kuchezewa (manipulation). Katika hatua hii, wale wanaoshikilia madaraka au wenye nguvu na sauti katika nchi kwa heri au shari, huutumia ushirikishwaji watu kama mbinu ya  uenezi habari na ujengaji mahusiano na watu kwa dhati au kwa unafiki.

Katika hatua hii, watu watakusanywa au wataunganishwa pamoja; wakaahidiwa hiki au kile; wakati mwingine wakitolewa kwenye rutuba na kupelekwa jangwani, wakatoka kwenye neema na kuwekwa kwenye dhiki na kisha mwisho wa yote  wale waliowapelekea huko wasiwape uongozi wala msaada wowote wa maana.  
       
 Ni katika hatua hii ambayo tunaona badala ya viongozi kwenda kuishi, kukaa na kupanga pamoja na wananchi ushirikishwaji wao mia kwa mia, wanasiasa mbalimbali na viongozi kwa ujumla huenda kuwaona wanavijiji kama vile wanavyokwenda kutembelea wanyama kwenye mbuga za utaliii. Kufika na kuondoka kwao hakubadili chochote zaidi ya kuwepo mabaki ya pilau, vinywaji na mapambo ya wao kufika na kuondoka.

Pamoja na kujulikana kwamba watu wote wanastahili kuwa na mahitaji ya msingi kwa kusaidiwa na jamii kubwa, yaani, kila familia kuwa na nyumba, shamba,  elimu na mafunzo, afya na tiba, huduma mbalimbali za kijamii, ajira kwa wenye umri wa kuajiriwa, fursa mbalimbali za kijamii na kiuchumi, wanasiasa huingia katika wakaligeuza zoezi zima kuwa ni sanaa na usanii mtupu.

Hatua ya pili ya ushirikishwaji watu ni TIBA. Katika hatua hii maadili, desturi, imani na mitazamo ya wasiokuwa na nguvu na wasiokuwa nacho hufinyangwa na kuingizwa ndani ya utamdauni na mila za wale wenye nguvu na uwezo katika jamii husika.

Katka mbuga za wanyama au pembezoni ya migodi ya madini, ambayo wakazi wa maeneo husika walistahili kuwa wanahisa na wamiliki wa miradi inayozuliwa huko, watu  watafungwa macho kwa kujengewa zahanati, shule, kibarabara au kidaraja na hapo ndiyo ufadhili wa hao wanaovua utajiri wetu kwa mabomba kila siku ukawa umeishia.

Hadi kufikia hapa, mwananchi mara nyingi anakuwa haijui Katiba ya nchi; hajui haki zake; hajui wajibu wake wala fursa za uteuzi mbalimbali zilizoko mbele yake. Hili linasahihishwa na hatua ya nne, ambayo inaitwa KUTAARIFIWA . Angalau, sasa katika kutaarifiwa mwanakijiji anaweza kujuaa haki, wajibu na fursa alizonazo kijamii na kimaendeleo. Hii ni hatua ya mwanzo kabisa, katika ushirikishwaji kiukweli kweli watu katika uamuzi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo na masuala mengine yanayogusa maisha yao ya kila siku.

Hatua ya USHAURI kwa maana ya kwamba na yeye anakuwa ni mshiriki katika mazungumzo au mikutano inayohusu maendeleo yake na wanakijiji wenzake, huwa inazidi kumpeleka juu zaidi mwanakijiji kuwa na nguvu na sauti katika kile kinachofanyika katika jamii yake. Hapa anasikiliza ujumbe na mawazo ya viongozi au wabia wengine, lakini pia na yeye anapata fursa ya kuchangia, kukosoa, kuongezea au kukataa wazo fulani dhahiri bin shayiri.

Hatua ya KUTAFADHALISHWA kama neno lenyewe linavyojidhihirisha hufikia pale ambapo hakuna uamuzi wowote, achilia mbali utekelezaji wa jambo lolote hufanyika pasipo wanakijiji kuliridhia kwa umoja wao. Mathalani, wakazi wa Mkoa wa Mtwara hivi sasa wanapinga gesi kutoka Mtwara na kupelekwa Dar es Salaam, mabomba Dar es salaam. Wanataaluma wa ushirikishwaji umma wakihusishwa wanaweza kurejelea hatua zilizotangulia wakasahihisha na baada ya Wamtwara kushirikishwa na wao wenyewe wakaona faida au manufaa moja, mbili, tatu watakayoyapata na wabia wengine wakawatafadhalisha basi wanaweza kuridhia na tatizo hili likawa limepatiwa ufumbuzi wa muda. Nguvu na kujua sana kukitumika matokeo yake yanaweza yasiwe mazuri kwa Wamtwara na Taifa kiujumla.

Hatua ya sita ni UBIA, ambayo kwa kawaida inahusu wenye mamlaka au nguvu kupatana na wanakijiji au wananchi juu ya jambo fulani,hivyo kwa kiasi fulani watawala kuwaachia nguvu na mamlaka fulani wanakijiji au wananchi. Mgawanyo huu wa mwanzo wa mamlaka, lazima uwepo ili kuwawezesha wananchi siyo tu kuwa na kauli katika uamuzi bali kuanza kutafiti na kuchunguza kisha kuasisi njia mbalimbali zinazoweza kuwawezesha kuwa na mtaji wa kijamii, jambo ambalo ni muhimu katika maendeleo ya watu vijijini.

Aghalabu, mifano mingi inaonyesha kwamba wananchi wakishaanza kushiriki kwenye kufanza maamuzi na utekelezaji mipango basi hatua ya saba, yaani, KUKAIMU MAMLAKA AU NGUVU  ZA KIUTAWALA, hufikiwa fumba na kufumbua. Ni katika hatua hii, ambapo wengi wa wanavijiji huanza kujisikia kweli ni watu huru na wanaoweza kuamua mwelekeo wa maisha yao na siyo kama kule nyuma ambako huwaachia watu wengine kuamua jinsi maisha yao ya leo na kesho yatakavyokuwa.

Hatua ya nane UDHIBITI MAMLAKA AU NGUVU na wananchi wenyewe ndiyo hatua ya juu au kilele katika ngazi ya ushirikishwaji watu katika uamuzi na utekelezaji mipango yao ya maendeleo. Ili ushirikishwaji wa kweli uwepo vijijini ipo haja ya kuangalia ni kwa namna gani uongozi wa vijijini unaweza kuanzishiwa muundo na mfumo utakaorahisisha viongozi hao kupatiwa elimu na mafunzo huko huko vijijini wanakoishi na kufanya kazi zao. Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi zina mchango mkubwa kwa kuifanya kauli ya 'elimu ni mama wa kila kitu' kuwa ya kweli vijijini kwa kusaidia na kuwaunga mkono wale wote ambao kutokana na kazi au shughuli zao za kielimu zinawalazimisha kwa njia moja au nyingine kuanza kuwaamsha watu na kuwatia mori wa kutafuta elimu na maarifa mapya ili wabadili maisha yao.

Yaliyozungumzwa hapa siyo mageni. Yapo katika kumbukumbu za mikutano kati ya Benki ya Dunia na JMT; kumbukumbu za Azimio la Arusha; kumbukumbu za Vijiji vya Ujamaa Tanzania; na kumbukumbu za Madaraka Mikoani kama zilivyoandikwa kwa kutumia maandiko ya watu na taasisi mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia, IMF na Mwalimu Nyerere. Kilicho tofauti kwa wakati huu ni nyakati kubadilika lakini haja ya kufanya na kutekeleza hatua za msingi ili kuwa na dhati ya kuupunguza umaskini inabakia palepale.

Hii ina maana kwamba,  ninachokihubiri hapa ni kwamba haitawezakana  kamwe kwa Tanzania kuondoa umaskini vijijini bila ya wanavijiji kukubali umoja, kujitolea na kujitegemea kwa maendeleo yao; bila Serikali kuwawezesha wananchi kwa wananchi hao kunufaika na ardhi yao na maliasili nyingine za nchi. Bila ya Serikali kurahisisha wananchi kufikia hatua ya juu kabisa katika ngazi ya ushirikishwaji watu katika uamuzi na utekelezaji mipango yao ya maendeleo huko huko waliko iwe ni ngazi ya kijiji, kata, tarafa, wilaya au mkoa.

Moyo wa kujitolea, umoja na ujamaa, kwa maana ya wanavijiji kuishi kama ndugu na kufaana wakati wa shida na matatizo, kujitegemea na kutumia nguvu za wanavijiji wote wanaojiweza kupata ufumbuzi wa matatizo ya kiuchumi, kuzalishaji, kijamii na kimazingira bado ni sera na siasa inayohitjaika na iliyo na nafasi ya kuleta maendeleo vijijini  kwa haraka kuliko njia nyingine yoyote.
Source: Mwananchi Communication