MARA nyingi vijana hupata taabu sana katika suala la kuchagua
mchumba. Vijana wa kiume ndio hasa hupata wakati mgumu zaidi kwani jamii
imewapa wajibu wa kuanzisha mazungumzo yahusianayo na mapenzi. Hata
hivyo, vijana wa kike nao wanao wajibu wa kuchagua ili kuhakikisha kuwa
hawaanguki mikononi mwa mabazazi wa kuwalaghai na kuwatumia kwa raha za
miili yao kisha kuwaacha kwenye mataa.
Ni jambo la kawaida kwa vijana walio wengi, wawe wa kike au wa kiume,
kuangalia sura na mwonekano wa mtu. Lakini unapotafuta mchum
ba kwa malengo ya kuishi naye maisha yako yote kama mume na mke
haipendezi kuangalia tu mwonekano, maana Waswahili husema si kila
king’aacho ni almasi. Kwa sababu hiyo, hapa yatabainishwa mambo muhimu
ya kuangalia na kuzingatia katika suala hili.
1. UADILIFU
Pamoja na sifa zote za uzuri zinazoweza kubainishwa na kufanywa kuwa
vigezo vya uzuri wa mwanamke na mwanaume na hata zikatumiwa kumpata Miss
au Mr Tanzania, sifa kuu impasayo mtu anayefaa kuwa mchumba kuwa nayo
ni sifa ya uadilifu.
Mtu anapokuwa na uadilifu (pengine uaminifu), maana yake ni kwamba
tabia ya mtu huyu anayoionesha nje ndiyo tabia yake halisi na anapofanya
jambo jema analifanya kwa roho yake na si kwa unafiki.
Mtu anapokuwa mwadilifu ataheshimu maadili na kufanya wema, hata pale
inapokuwa rahisi kwa wengine kukengeuka na kufuata njia za mkato ambazo
mara nyingi si za halali.
Mtu mwadilifu pia huwa na sifa za ukweli na kujitolea kuwasaidia watu
wengine bila kujali faida – haya yote ni mambo muhimu ambayo mtu mwenye
kuwa nayo huwa na msingi wa ujenzi wa uhusiano imara na wa kudumu.
Watu wanaoweza kujivunia furaha ya kweli katika maisha yao ya ndoa,
ni watu ambao wamekutana wote wakiwa na sifa ya uadilifu ambayo
hujumuisha mambo mengi.
Zipo ndoa nyingi zenye furaha ya bandia. Furaha hii mara nyingi
hutokana na ridhiko la kimwili alipatalo mtu kutokana na kukidhiwa kwa
mahitaji yake ya kimwili yanayohusiana na haki za msingi za binadamu –
yaani chakula, mavazi na malazi. Lakini furaha ya kweli ya maisha ya
ndoa, watu hawaipati isipokuwa katika uhusiano ambao wenza
wamethibitishana kuwa waadilifu.
2. HEKIMA
Mtu mwenye uadilifu wa kweli, mbali na kuwa mwema kwa mwenzake, pia
huhakikisha anakabiliana kwa busara na hekima na matatizo yote
yanayoweza kusababisha kuyumba kwa uhusiano, hususan yale yaliyo nje ya
uwezo wake.
Uzoefu unaonesha kuwa wapenzi, hususan wanandoa walio katika uhusiano
wa muda mrefu wanaoendelea kufurahia unyumba wao si wale ambao
walipendana kwa mvuto na wala hawana mambo mengi ya asili
yanayowaunganisha kuliko wale wanaotengana. Lakini la muhimu ni kwamba
watu hawa huwa wamejifunza jinsi ya kukabiliana kwa hekima na matatizo
yanayojitokeza, hususan yale yanayotokana na tofauti zao kimtazamo.
Ukiachilia mbali sifa ya uadilifu, watu hawa huwa wamejifunza
kukabiliana na matatizo kuhusiana na uzazi na ulezi wa watoto, uhusiano
na ndugu, jamaa na marafiki, suala la ngono, fedha na maisha ya unyumba
kwa ujumla.
Habari njema ni kwamba uadilifu na hekima ni mambo ambayo mtu yeyote
anaweza kujifunza na kisha kufanyia kazi. Ndiyo maana wanandoa
hufundishwa kabla ya ndoa na hata wanapokuwa tayari wameoana huendelea
kuhudhuria semina za kidini na kijamii kwa ajili ya kujiimarisha.
Kwa hiyo, kama mume/mke wako mtarajiwa anaonekana kuwa na utayari wa
kujifunza kuhusiana na jinsi ya kuishi na mtu wa jinsia nyingine, ana
nafasi kubwa ya kuwa mke/mume mzuri baadaye.
3. UPOLE
Mfalme Suleiman katika mojawapo ya semi zake za hekima alisema
mwanamke mpumbavu huibomoa nyumba yake kwa mikono yake. Yamkini ndivyo
ilivyo pia kwa mwanaume mpumbavu, maana upumbavu haujengi.
Siku zote kitu kinachovunja uhusiano wa kindoa si makombora ya
nyuklia, bali ni ulimi. Kwa kadri mtu anavyoutumia ulimi wake anaweza
kuijenga au kuibomoa nyumba yake.
Katika kumwangalia mtu ambaye unaweza kujenga naye nyumba ya kudumu,
ni vema kumchunguza na kuhakikisha kuwa si mtu mwenye kupenda kurefusha
maneno, maana hakika huyu atasababisha ugomvi mara kwa mara na uhusiano
hautadumu.
Wapo watu ambao ndoa zao zina sifa ya ugomvi na karibu kila mtu
anafahamu na hata wamekuwa kero kwa ndugu, jamaa na majirani zao, mara
kwa mara wakiwaamsha watu usiku wa manane wakitafuta suluhu.
Mara nyingi wanaume ndio huanzisha ugomvi, lakini ugomvi huwa na
nguvu zaidi kama mwanamke ni msemaji. Dawa ya kuzuia ugomvi usiokuwa na
mpango ni kupunguza maneno na kuepuka kutafuta ushindi katika ubishi.
Lakini kinga ya tatizo hili ni kuepuka kujiingiza katika uhusiano na mtu
ambaye umejihakikishia kuwa si mwingi wa maneno.
Bahati nzuri, jamii huwatambua wanawake/wanaume ambao wanaweza kuwa
wake/waume bora baadaye kwa hiyo ni wajibu wa mtafutaji kuhakikisha kuwa
anafanya uchunguzi wa kina kabla ya kujitosa kwa mtu ambaye baadaye
atamtaabisha.
Mwanandoa aliyeifahamu vema dhana ya ndoa – kwamba ni maisha ya
kuvumiliana na kuchukuliana, hufahamu ni wakati gani wa kusema na wakati
gani wa kukaa kimya. Mtu huyu pia hufahamu njia nzuri na salama ya
kujiondoa kwenye tatizo anapoona mwenzake anaelekea kubaya, ili hatimaye
uhusiano wao uendelee kuwa salama japo wao wanaweza kuwa wamekwaruzana.
Mtu huyu mwenye upole hujiweka katika mkao wa upatanishi na
huhakikisha kuwa kila mjadala mkali unapita na kumalizika salama. Ni
wazi kuwa katika kutafuta, kama hukukurupuka, utamwona mtu mwenye hulka
hii – upole.
4. MVUTO
Hisia za mvuto wa kimapenzi ni muhimu katika kujenga uhusiano. Mtu
mmoja akauliza, ni yupi bora – yule anayenivutia sana au yule
anayenipenda sana? Maisha ni ya ajabu sana. Huwa inatokea kuwa mtu
unayevutiwa naye sana yeye havutiwi nawe, bali anavutiwa na mwingine
ambaye naye hana mpango naye!
Haya ndiyo maisha. Uzoefu unaonesha kuwa asilimia kubwa ya watu walio
katika ndoa hawajawaoa/kuolewa na watu waliokuwa wakiwapenda sana enzi
za ujana wao, au wale waliotimiza ndoto za ujana wao. Bahati njema
miongoni mwa wanandoa hawa wapo wale wenye ndoa imara sana.
Mvuto wa kimapenzi ni muhimu sana, lakini watu husema maji yakisema
usininywe yajibu kuwa wewe pia huna kiu nayo. Japo inaweza kuonekana
kama ni aina ya ‘sizitaki mbichi hizi’ lakini si vema kujisumbua na mtu
asiyekupenda.
Badala ya kujihangaisha na mtu asiyekupenda, kaa chini na umsubiri
anayekupenda hata kama huhisi kuvutiwa naye sana. Baadaye utamzoea na
maisha yatakuwa mazuri, kisha utajiuliza baadaye yule aliyekuringia
alikuwa na nini cha ziada?
Lakini iwapo mambo mengine yote yatakwenda sawa, ni vema na muhimu
kabisa kuhakikisha kuwa mtu unayepanga kuwa naye maisha yako yote ni mtu
anayekuvutia kimwili na kiakili, maana vinginevyo unaweza kupata sababu
ya kukidhi kiu yako nje – jambo ambalo si maadili mema katika ndoa na
maisha.
NI MUHIMU KUWA MAKINI
Katika nyakati za ujana, watu wengi hubabaishwa kwa mengi. Vijana wa
kiume hubabaishwa na sura, maumbile na pengine rangi na kusahau mambo
muhimu yaundayo orodha ya sifa za mke mwema.
Kwa upande wao, vijana wa kile pia waweza kubabaishwa na pesa,
maumbile, sura, utanashati, umaarufu au kuchoshwa na shinikizo la umri,
hivyo kujikuta wakijitumbukiza kwa wanaume wasio na sifa za waume
wazuri.
Lakini tukirejea kwenye msemo wa zamani kuwa uzuri si hoja bora
tabia, ni wazi kuwa tutafikia mahali tutajenga mahusiano imara na
yasiyotikiswa na sunami zozote za kimaisha. Ilimradi tu uhakikishe kuwa
mtu mwenyewe anakupa mvuto kimapenzi, maana vinginevyo kutakuwa hakuna
maana.