Habari za hivi punde zinaarifu kuwa
ofisi ya rais Yanukovych nchini Ukrain imetoa taarifa inayosema kwamba mwafaka
umefikiwa katika mazungumzo ya usiku kucha kati ya serikali ,upinzani na
waakilishi wa Muungano wa Ulaya na Urusi.
Taarifa hiyo hata hivyo haikutoa
maelezo zaidi kuhusu makubaliano hayo ingawa ilisema kuwa pande zote zitatia
saini makubaliano yenyewe
Duru zinasema kuwa Rais Yanukovych
amekuwa akikabiliwa na shinikizo apange uchaguzi wa mapema pamoja na mageuzi ya
kikatiba.
Umoja wa Ulaya umekubali kuwawekea
vikwazo viongozi waliopanga ghasia zinazoikabili Ukraine kwa sasa.
Uamuzi huo uliofanyika mjini
Brussels, Ubelgiji umejiri baada ya watu kadhaa kuuawa mjini Kiev, katika siku
ambayo ilishuhudia umwagikaji mkubwa zaidi wa damu tangu uhuru wa Ukraine zaidi
ya miaka ishirini iliyopita.
Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni
wa Italia, Emma Bonino, amesema vikwazo hivyo vinavyojumuisha vya usafiri na
kupiga tanji mali za wahusika na kwamba vinawalenga wale waliohusika na mauaji
ya waandamanaji.
Ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Kiev
unajaribu kuwapatanisha viongozi wa upinzani na rais Victor Yanukovych ili kuleta
amani na pia kushawishi taifa hilo kuandaa mapema uchaguzi uliopangiwa
kufanyika mwaka ujao.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa ,
Ban Ki-moon amesema hali nchini Ukraine ni ya kutamausha:
Wito huo umetolewa vile vile na
waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry ambaye ametaka
vurugu kusitishwa nchini Ukraine akisema kuwa watu wa taifa hilo wanastahili
kuwa na hali bora kuliko kile alichokitaja kuwa maafa na mateso yasiyofaa
ambayo yameshuhudiwa katika barabara za mji mkuu, Kiev.
Haijabainika ni watu wangapi
waliouwawa katika vurugu za Alhamisi lakini wizara ya Afya inasema tangu
Jumanne, watu sabini wameuawa na zaidi ya 570 wamejeruhiwa.
SOURCE: BBC-Swahili
No comments:
Post a Comment